Thursday, October 7, 2010

Muungwana akivuliwa nguo, huchutama!

Na Hussein Wamaywa

Mwayaona Biti  Kuishiwa alikuwa alikuwa mshauri na msiri wake mkuu, ilikuwa aghalabu kwa Shufaa kupata tatizo na kutulia tuli pasipo kumfuata bibi hyuo mcheshi na na mwenye busara ambaye alikuwa akiishi nae pamoja pale Unga Limited Arusha.
Jumamosi hii ilikuwa ndio kwanza Mwayaona ametoka kuweka vitumbua vyake nje, akamuona Shufaa akimsogelea kwa sura iliyosawijika na kupoteza nuru. Akasimama na kumpokea.
“Karibu mwana, karibu mwali wangu!”
Hii huwa salamu yake ya Kawaida ambayo Shufaa tayari alikuwa ameizoea. Tofauti na siku nyingine, siku hii Shufaa alishindwa kuijibu badala yake machozi yaliyokuwa yakifanya fujo katika macho yake yakateleza na kuangukia mashavuni, hali midomo ikitengenezwa kuachia kilio.
Halafu kilio cha haja kikamuanguka.
Nguvu zikamuishia, na isingekuwa Bi Mwayaona kumdaka angeanguka vibaya. Na yale mawe yaliyokizunguka kibara za cha nyumba ile, saa hizi tungekuwa tunaongea habari zingine.
Akiendelea kuangua kilio, Mwayaona alimsaidia Shufaa kutembea, akamkaribisha ndani na kochi likamlaki. Akamlegeza nguo zake na kumfuta machozi. Akamwacha apumzike na kutoka nje. Aliporudi alikuwa na kinywaji fulani cha baridi, kinywaji kipenzi cha Shufaa.. Alimkuta ameshanyamanza na alikuwa akisina sina kwa kilio.
“Mwanamke anasifiwa kwa mapenzi!” Akamwambia kwa utani akimtengea kinywaji. “Mwanamke anasifiwa kwa kummiliki na kumdhibiti mumewe! na katu hasifiwi kwa kulia! Nyamanza mwali wangu unieleze hicho kichangiacho kukukosesha raha!” Alishamaliza kumtengea na sasa alikuwa ameketi  sambamba nae.
Shufaa akaangua kilio upya. Tena kilio cha kwikwi.
Hili likamshtua tena Mwayaona, akamsogelea na kuketi ubavuni mwake. ‘Pengine ana tatizo kubwa! Pengine amefiwa!’ Akawaza akimbembeleza zaidi. Ilikuwa ni dakika nyingi baadae ndipo Shufaa aliponyamanza na kuanza kumueleza.
“Nina matatizo bibi! Tena matatizo makubwa!”
“Matatizo ni kawaida kwa kila Mwanaadamu!”
“Nafahamu Bibi, lakini ya kwangu yamezidi. Kana kwamba nililetwa duniani nije kuteseka na kuumia.”
“Waweza kudhani hivyo, lakini kila ukiona kwako kunaungua basi ujue kwa mwenzako kuna tekeketea!”
“Kweli?!”
“Eeeh! Angalia watoto wa mitaani kwa upande mmoja, kisha magereza kwa upande miwingine, halafu tembelea hospitalini. Zile hospitali za sie akina yahe, kama hiyo haitoshi sikiliza Njia Panda ya Redio Clouds FM kila jumapili jioni. Unaweza kudhani Mungu amekupendelea kwa kukupa hilo tatizo ulilonalo!”
Maneno yakamuingia Shufaa.
Akashusha pumzi na kufuta machozi, tena akapata hata nguvu ya kunywa kinywaji chake. Moyoni Mwayaona akjisifu kwa kuirejesha furaha ya binti huyu, shoga yake kipenzi. Akakaa vizuri zaidi.
“Haya niambie mpenzi, kipi kikusikitishacho?”
“Ni kuhusu Ramla Bibi!”
“Ramla  Maulid Mwinyihumbe?!” Mwayaona Akataka uhakika. Shufaa akakubali kwa kutikisa kichwa.
“Si dada yako yule? Kwa nini awe chanzo cha kupotea kwa furaha yako kiasi hiki?”
“Sio Dada yangu yule!”
“Amah!” Mwayaona akashuka na kushangaa, akaongeza. “Lakini kila mtu anajua kwamba Ramla ni dada yako, dada mzazi, dada wa toka nitoke!”
“Wote huo sio ukweli bibi”.
“Kumbe ukweli ni upi?”
Mwapwani akatabasamu. Akakipeleka kinywaji chake mdomoni na kukitua chini. akaketi vizuri na kumtazama Bi Mwayaona kwa jicho la upendo. “Nadhani itakuwa vyema nikikupa historia yangu” Akasema kwa mnong’ono mzito “Historia ambayo sikuwahi kumwambia yeyote kabla…”

*          *          *
Msikiti wake ulijengwa pembeni kabisa mwa Bahari ya Hindi. Pengine ni hili lilioufanya Msikiti huu uitwe wa pwani. Ulikuwa wake kwa sababu kuu mbili. Kwanza alikuwa amechangia zaidi ya nusu ya ujenzi wake. na pili hakupenda kusali kaatika msikiti mwingine wowote anapokuwa nyumbani kwake Zanzibar. Kubwa zaidi ulipewa jina lake ‘Al - Masjidi Maulid.
Alfajiri hii akiwa na safari muhimu ya Bara alikokuwa na vitega uchumi vya haja; mara alipomaliza kusali tu, Mzee Maulid Mwinyihumbe hakusubiri zaidi. Aliondoka haraka huku akiwaacha wenzie wakiendelea na umaliziaji wa ibada. Nje ya Msikiti akayaweka makubadhi yake miguuni, koti akalivuta libane vizuri kumsitiri na kibaridi kikali cha asubuhi, akaivuta kanzu yake juu kidogo ya magoti ili imuwezeshe kutembea haraka zaidi.
Upesi upesi akavuta hatua kuelekea nyumbani kwake. Dakika chache tu toka aanze kutembea akashtuka, moyo ukafanya puuh sambamba na kuongeza mapigo huku nywele zikimsimama. Akatega sikio na kusikiliza vizuri, miguu ilishatoka katika makubadhi tayari kwa kutimua mbio!
Naam! Akasikia tena.
Safari hii kwa usahihi zaidi. Masikio hayakuwa yamemdanganya awali. Kilikuwa kilio cha mtoto mdogo na tuseme mchanga. Ujasiri ukamshika, akausahau umuhimu wa safari yake ya bara, taratibu akaanza kufuatilia kule kilio kilipotokea ambacho kilikuwa kikingali kikiendelea!
Hakuchukua muda kukiona kitoto kizuri kichanga kilichokuwa kimevingirishwa ndani ya khanga moja nyepesi ya India iliyoandikwa dunia uwanja wa fujo. Lakini kutokana na giza, Mwinyihumbe hayaona maandishi hayo.
Alichokifikiria haraka akilini mwake ni baridi. Kama yeye mwenye kizibao, kanzu, koti, kikoi na kofia alikuwa akisikia baridi, vipi kwa kichanga kile kilichoviringishwa ndani ya ki-khanga kimoja?!
Haraka akakiokota na na kukifunika vizuri, akavua koti na kukifunika barabara, akakibeba vizuri na kuondoka nacho kikiwa kimenyamanza “Masikini pengine baridi ilikizidia!” Akawaza kwa huruma akikaza mwendo zaidi. “Loh! Kingefariki hivi hivi! Haki ya Mungu binaadamu tuna dhambi sana!”
Akahitimisha akichnganya miguu zaidi.
Nyumbani, mkewe alimlaki kwa mshangao usiosemeka. Mzee Mwinyi akamueleza kila kitu tokea mwanzo mpaka mwisho! Bi Hanifa Mzeru  mkewe Mwinyihumbe akashusha pumzi ndefu.
“Umefanya vizuri mume wangu. Mimi nadhani itakuwa vyema kama tutampeleka katika vituo vya kulelea watoto yatima. Ma’mkubwa  Mwanahamisi aliwahi kunimbia kwamba kuna vituo vya kutosha vya…!”
Akaukatisha usemi wake baada ya kumuona mumewe akimtazama kwa jicho kali.
“Una maana gani kusema hivyo? Kwani sisi hatuna uwezo wa kumlea?” akamuuliza kwa ukali.
“Sio hivyo mume wangu”
“Kumbe?”
Bi Hanifa akasita tena kwa muda
“Ndugu zake wanaweza kuja kumtafuta baadae. Watatushtaki kwa kwa kumlea mtoto wao bila ridhaa yao, watatuona wezi!”
“Kwa hiyo bora tungemuacha malaika huyu wa Mungu akafa?”
“Ndiyo maana nashauri tumpeleke anakohusika ili...!”
“Sikiliza mke wangu!” akamkata kauli tena “Sikiliza mama Shomari,” Akasisitiza na kuendelea kwa sauti yenye uzito wa pekee, “Mtoto huyu ni wetu. Mtoto huyu ni wangu kwa kila hali, ni zawadi maalum toka kwa muumba. Sitampeleka popote, badala yake nitamlea na na kumpa kila kinachohitajika mpaka atakapokuwa na uwezo wa kuendesha maisha yake. Siwezi kufilisika kwa kumlea mtoto huyu mmoja tu! Siwezi. Na nitamlea! Hakika nitamlea. Hakuna wa kunizuia kuhusu hili!” Akaamua na kuingia nae ndani.
Bi Hanifa akabaki amejiinamia pale sebuleni alfajiri ile akimfikiria mumewe na maamuzi yake.
Alimjua Maulid Mwinyihumbe vizuri sana toka akiwa hohe hahe alipomuoa miaka ile ya kisogoni. Akiamua kitu ameamua. Usidhani atayakana maamuzi yake. Kilichokuwa kikimkera Bi Hanifa ni kule kutoshirikishwa katika maamuzi mbalimbali aliyodhani kuwa yalikuwa yakimuhusu ndewe na sikio.
Ilikuwa hajapita hata miaka mitano toka waliposikiliza redio moja binafsi iliyokuwa ikirusha maelezo ya mitaani wanaoishi katika mazingira magumu. Walijikuta wakivutwa na maelezo ya binti mmoja mwenye umri wa miaka mitatu aliyetupwa toka akingali mchanga na wazazi wake. Wakamuhurumia sana.
Siku ya pili Maulid mumewe akawa amerejea na yule mtoto wa kike aliyejulikana kwa jina la Ramla Rashid.
“Huyu nae ni nani?” Mkewe akamuuliza.
“Ramla! Yule binti tuliyekuwa tukimsikiliza jana redioni!”
Machozi yakamtoka Hanifa. “Pole sana mwanangu” akasema akimpakata na kumkumbatia katika hali ya upendo iliyopatiliza. Hakika alipata mapenzi ya kweli. Katika hali hii, Ramla alionyeshwa upendo wa aina zote uliompatia faraja za aina yake. alikula wali, akacheza muziki na watoto wenzake, akaangalia TV na kuchezea midoli. Alipochoka alipewa kitanda na kulala.
Usiku ndipo Maulid Mwinyihumbe alipomueleza mkewe kwamba binti huyo ataishi nao hapo nyumbani na wataishi naye kama mtoto wao. Ingawa hakuwa ameyapenda maamuzi hayo, Bi Hanifa alilazimika kukubali kwa vile alikuwa ameyasikia matatizo ya Ramla kwa masikio yake na kuyashuhudia jinsi yalivyo makubwa sana.
Miaka mitatu baadae Ramla akaanza shule akiwa amebadili ubini na kutumia jina la Ramla Maulidi.
Halafu akamleta kijana mwingine kutoka kusikojulikana!
Naye alielezwa kama mwenye matatizo ya moyo na alihitaji msaada wa kupelekwa India kwenda kutibiwa. Hivyo mzee Maulid ambaye hakuwa na fedha wakati huo, akaamua kukaa naye hapo nyumbani wakati akitafuta fedha za kumpeleka kijana huyo huko India.
Hili Bi Hanifa alilipinga waziwazi tena mbele ya mumewe na Hamis Abdalaah, huyo  kijana aliyekuwa akitafuta msaada. Na katika kuonyesha hasira zake akaamua kufungasha kila kilicho chake na kurudi kwao.
Hasira zake zilipungua miaka miwili baadae! Aliporudi kwa m,umewe alimkuta ameshaoa wake wengine wawili zaidi!! Mmoja alikuwa amefariki mapema tu baada ya kuolewa, akamuachia mtoto mmoja ambaye Bi Hanifa alilazimika kumlea. Hanifa alilia sana lakini mwisho wa siku akawa amejifunza kwamba dawa ya tatizo siyo kulikimbia bali kulikabili na kulitatua. Mwanzo alikuwa pekee. Sasa amemkuta mke mwenzie na watoto wawili zaidi. Hakuwa na jinsi, akaanza maisha upya.
Bahati ilikuwa yake kwa vile Mwajabu Mohamed, huyo mke mwenzie alipenda sana kuishi shambani kule kwenye viunga vya minazi na karafuu. Hivyo Hanifa akabakia kuwa mke pekee hapo nyumbani.
“Sasa leo tena kimeletwa kichanga, mjadala hakuna! Ni mtoto wa  Maulid Mwinyihumbe baasi! Shenzi type!” Akafyonya akisimama na kumfuata mumewe ndani. Alimkuta amekivinringa khanga zake, amekitandikia taulo na kulala nacho kitandani ndani ya chandarua.
Akamtazama mumewe kabla kutikisa kichwa kwa masikitiko na kupanda kitandani. Akamgusa begani kwa upendo. Muewe akageuka na kumtazama
“Kumradhi baba Shomari,” akaomba.
“Hujanikosea mke wangu. Najua bado hunielewi kwa vitendo vyangu laaziz. Lakini iko siku utanielewa mpenzi; unatakiwa uwe mwema kwa mwenzako leo, kwa kuwa hujui kitu gani kitatokea kesho” Akatua kupitisha mate kooni. Bi Hanifa akamsikiliza kwa umakini zaidi.
“Wewe ni mke wangu, ni mama wa wanangu. Na kumbuka siku zote maisha ni safari ndefu na yenye vitimbwi vingi, tena ni safari usiyoweza kutabiri mwisho wake ukoje. Kwa maana hiyo hata siku moja usijiongopee kwa asilimia mia moja kuwa wanao wakina Salumu, Johari na Busara wanaweza kuja kukusaidia baadae. Pengine ni hawa hawa akina Hamisi na Fatuma ndio wakaja kukuokoa wakati utakapokuwa huna mbele wala nyuma. Wakati huo wanao washakuwa manunda kwisha kazi!”
“Samahani,” Hanifa akawahi kwa hasira baridi, “Usiwafananishe wanagu na manunda!”
“Basi mke wangu, tulale tusijeitia doa siku hii ya baraka iliyoanza vizuri!”
“Tulale?!” Alikuwa Hanifa kwa Mshangao “Wakati una safari ya bara?”
“Ni kweli, lakini nitaondoka baadae sana!”
Ukimya mfupi ukapita. Bi Hanifa akajaribu kulala akashindwa. Baadae akasaili tena.
“Jina lake nani?”
“Mtoto? Hata nilikuwa sijafikiria. Sijui nimwite nani vile…”
Kikapita kimya kingine cha muda “Kwani…” Hanifa akakivunja kimya hicho. “Ni mtoto wa kike au wa kiume?”
“Wa kike!”
“Unaonaje ukimwita Shufaa, jina la dada yako mke wa Muharami? Pengine akawa mkarimu na mwenye upendo kama Shufaa mwenyewe. Si wanasema majina huakisi na kuzibeba tabia za watu wake wa awali.”
“Eti enhe?” Mwinyihumbe akakurupuka kama aliyetoka usingizini, uso wake ukichanaua kwa tabasamu maridhawa. “Vyema aitwe hivyo. Litakuwa jina zuri ajabu, Shufaa Maulid Mwinyihumbe. Aitwe hivyo!” Akahitimisha. Safari hii sauti yake ikiwa na uhai. Ilikuea kama aina fulani ya amri kama sio mamlaka.
Walikubaliana kumlea vyema kwa mapenzi yao yote wakimfanya kuwa sehemu ya watoto wao.
Watoto wake walipomuuliza kesho yake mtoto mchanga katokea wapi, mama yao akawaficha yakiwa ni maagizo ya kutoka kwa mume wake Mwinyihumbe. Lakini Shomari na Johari ambao walikuwa wakubwa zaidi kiumri walipombana mama yao mchana akashindwa kuwaficha na kuwaeleza kila kitu.
“Shit!” Shomari akaguta kwa hasira “Baba bwana, kishageuza mahala hapa kama Orphan Children Care! Mimi atanikoma!”


*          *          *
Huu ulikuwa mwanzo wa maisha ya Shufaa katika himaya ya Maulid Mwinyihumbe. Shomari na Johari hawakumpenda hata chembe. Alianza kupata misuko suko hata kabla hajatambaa. Mzee Maulid alipoligundua hili aliwakemea na kuwaadhibu wanae vizuri sana. Hata alipogundua kwamba wanaendelea akaamua kuwapeleka shule za mbali kusoma ambapo walikuwa wakirudi mara mbili kila baada ya mwaka mmoja.
Miaka ikayoyoma Shufaa akinyonya maziwa ya kopo huku akionyesha dalili za kuwapenda wote, ingawa waliompenda kwa dhati walikuwa wawili tu, Ramla na Hamis Abdalaah.
Na muda ulipojiri akaanza kusoma ‘vidudu’ pale Dhahabu Children Care. Alikuwa na akili kama mchwa. Akili yake ilikata kama wembe! Hili likamfanya awe kipenzi wa kila mtu.
Hiyo ilikuwa julai ya elfu moja mia tisa themanini na tatu.

*          *          *         
Miaka ikasogea taratibu. Shufaa alishafika darasa la tano na Ramla alikuwa kidato cha kwanza. Hamis alishakwenda India mara mbili na kupata matibabu ya haja na alikuwa mbioni kupelekwa mara ya mwisho kumalizia hatua za mwisho za kuponyesha maradhi yake kabisa.
Maulid Mwinyihumbe alishaweza kuidhibiti nyumba yake, watoto wake halali na wale wa hiyari. Ukiondoa Johari na Shomari ambao bado walikuwa wakiendelea na masomo yao nje ya Zanzibar, wengine wote waliishi kwa maelewano mazuri yaliyopendeza.
Siku moja wakati wa likizo, Mzee Maulid alirejea nyumbani mapema kuliko ilivyo kawaida yake na kukuta Ramla na Shufaa wakipigana. Damu zilikuwa zikimtoka Ramla puani, wakati Shufaa alikuwa ndani ya gagulo tu (wenyewe wanaziita under ware) baada ya nguo zake kuraruliwa na Ramla.
Kiwajihi Ramla alikuwa mwembamba na alijaaliwa umbo dogo dogo la kijapani kiasi cha kubatizwa jina la utani la Japanese. Umbo hili alilifanya imara kwa mazoezi na kazi nzito na zinazohitaji nguvu.
Hali ikiwa hivi kwa Ramla, kwa Shufaa hali ilikuwa tofauti. Alipanda juu kisukuma na kukatika kibantu haswaa. Walipotembea barabarani, Shufaa alionekana mkubwa kwa Ramla. Kitabia pia walikuwa na tofauti. Ramla alikuwa chakaramu na asiyekubali kushindwa kabisa wakati Shufaa alikuwa mpole wa maneno na vitendo. Hakuna aliyejua hasa waligombania nini.
Waliporejea tu kutoka tuisheni, Ramla alikuwa akimtukana na kumfokea Shufaa isivyo kawaida. Alimtukana na kumfokea sana licha ya mama yake Bi Hanifa, Salim, Busara na kaka yake Hamis Abdalah kumtaka amsamehe; bado Ramla aliendea tu kubwata.
Yalipomshinda Shufaa akaamua kujibu. Ikawa kosa, Ramla akaanza kumshambulia Shufaa kwa kumnyuka makofi kadhaa na Ramla alipomrudishia kujitetea ndipo ‘ndondi’ hizi zilipoanza rasmi. Hamisi na wenzake walikuwa wamejaribu kusuluhisha bila mafanikio, wakamua kuwaacha. Ni katika wakati huu mzee Maulid alipoingia.
“Mnapigana?!!” Maulid akabwata mara moja tu kwa sauti kali. Kwa aibu Ramla akaiachia shingo ya Shufaa na kuanza kulia. Shufaa nae akaanza kulia.
“Ramla na Shufaa mnapigana?!” akarudia tena machozi yakimtoka. Akaingia ndani na kuangua kilio. Kilio kikuu, kilio kilichowatia simanzi wote.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mzee Maulid kulia hadharani. Kila mtu alijikuta akitokwa na machozi.
Kama walioamrishwa, Ramla na Shufaa wakakimbilia vyumbani mwao kujiswafi ambapo kila mmoja alirejea baadae akiwa amebadili nguo, wote wakaelekea sebuleni. Bado Mzee Maulid Mwinyihumbe alikuwa analia akiweweseka taratibu.
 “Shufaa na Ramla mnapigana! Mnapigana! Mnapigana!”
Hanifa na wanae walikuwa wamembembeleza bila mafanikio, sasa walikuwa wamekaa pembeni na kulia. Ramla akijisikia vibaya kuwa chanzo cha vilio vya wote hawa.
Akijiamini kwamba alikuwa mtoto kipenzi kwa Mzee Maulid Mwinyihumbe, Shufaa alisimama na kumsogelea baba yake huku amepiga magoti, machozi yakiendelea kumtoka “Baba … tumefanya kosa, tunajua tumekuumiza sana, tafadhali acha kulia. Dada Ramla ndiye mchokozi. Tusamehe baba, ukiendelea kulia sisi tunaumia, tutakosa baraka zako. Tusamehe baba tunakiri kwa dhati”
Ikamgusa. Akaacha kulia na kuwatazama wanawe hawa wa hiyari. Walikuwa wamepiga magoti mbele yake, vichwa wameviinamisha ikiwa ishara ya kukiri na kuomba radhi kwa dhati.
“Kakaeni! Kakaeni wanangu,” Akasema baada ya kupenga kamasi na kufuta machozi. Akakaa vizuri na kuwatazama, akawauliza. “Mnaweza kunieleza sababu za kupigana kwenu? Mbona kila kitu mnapata?”
Ukimya ukatawala kwa muda.
Shufaa alipotaka kujibu, Maulid akamzuia.
“Siku moja asubuhi, nilikuwa nikisikiliza redio…” Akaanza hivi, ambapo alieleza kisa chote cha Ramla. Alipomaliza wote walikuwa wakimtazama kwa mshangao pasi na kuamini kile ambacho masikio yao yalikuwa yamekisikia. Baadhi wakisikia kwa mara ya kwanza kabisa.
“Na siku nyingine nilikuwa nikitokea Msikitini alfajiri…” Hapo tena akaeleza mkasa wa Shufaa. Alipohitimisha Ramla alikuwa akilia na kumuomba mdogo wake na baba yake wamsamehe. Shufaa pia akilia akitaka Dada yake na baba yake wamsamehe. Baba kadhalika akitaka wanawe wamsamehe, pengine kwa kuwapa siri hiyo.
Kilio kikaendelea. Hamis Abdalah akawaonea huruma watu hawa ambao kila mmoja alikuwa akimuhurumia mwenzake. Salum, Busara na mama yao pia, walikuwa katika hali hii.
“Msipigane tena maishani. Nyinyi sio watoto wangu ingawa ni wanangu. Hawa pia sio ndugu zenu ingawa ni wenzenu. Mnapaswa kupendana sasa, wewe Ramla huyu ni mdogo wako, na wewe Shufaa huyu ni dada yako.
Mshikamane na kuheshimiana. Mimi nikifa leo au kesho muishi vizuri. Msitegemee kama hawa…” Akawasota wanae, “Wanaweza kuwakumbuka katika urithi. wanaweza kukutimueni kwa mangumi na mateke licha ya kwamba mnafahamika kama wanangu. Msipopendana ninyi mnaofanana nani atawapenda?”
Akatua na kulia upya.
Shufaa na Ramla wakashindwa kuvumilia na kumvamia baba yao. Wakamkumbatia kwa nguvu na kulia nae pamoja. Halafu Hamisi akafuatia, wanawe na  mke wake nao wakajiunga. Walidumu katika hali hiyo kwa muda na walipokuja kuachiana, Shufaa na ramla wakala kiapo na kulishana yamini ya kuishi pamoja mpaka kifo kitakapowatenganisha.
Kilikuwa kiapo cha dhati na kuanzia hapo mapenzi yakawa ya dhati baina ya ndugu hao wawili. Hata Hamis alipoondoka kwenda India kwa mara nyingine tena, naye alikuwa na uhakika kwamba ni kifo tu ndicho kitakachowatenganisha ndugu hawa.

*          *          *
Halafu ikajiri siku ya siku, siku isiyo na jina. Siku ya balaa.
Mzee Maulid Mwinyi Humbe, mke wake Hanifa na mke mdogo Mwajabu Mohamed na watoto wao wanne walikuwa wamekwenda Mafia kuhudhuria harusi ya swahiba wake mkubwa Abdul Mohamed almaarufu  2man
Ni vile walivyoshibana na Abduli tu ndiyo iliyopelekea Maulidi Mwinyihumbe kupeleka familia yake nzima katika harusi hiyo. Nyumbani walibakia Ramla, Shufaa kwa sababu za kimasomo; na mtoto mmoja wa Bi Mwajabu ambaye afya yake haikuwa nzuri.
Safari ilikuwa nzuri, harusi ilikuwa nzuri pia. Ila safari ya kurudi ndio ikawa mbaya. Boti lilipigwa kumbo na dhoruba kubwa, likapinduka baada ya mashine kuzimika wakati wa tufani.
Hakuna aliyesalimika! Habari zilipofika Unguja nyumbani kwa mzee Maulid, shufaa na mdogo wake walizimia mara kadhaa mshtuko na uchungu, wasijue wataishi vipi bila baba yao mpendwa aliyewapenda ukomo upeo wa kuwapenda.
Mazishi yakafanyika baadae kwa maiti chache zilizoonekana. Siku chache za matanga zikaisha. Kilichofuatia ni Shomari na Johari waliokuwa shuleni ambao walikuwa wamerejea msibani; kuwafukuza Shufaa na Ramla ki-mbwa, ki-nguruwe!”
Sikumbili tatu za kutangatanga mitaani zikakatika. Hatimaye wakapata nyumba nyingine kule michenzani. Biashara ya shule kwa Ramla ikaingia mashaka makubwa.
Ramla akaingia mitaani kama dada poa, hali Shufaa akiuza bidhaa ndogo ndogo. Wakawa wameuanza mkondo mpya wa maisha kwa staili ya ina yake.
Miaka ikakatika, Ramla akawa mzoefu kwenye udada poa. Shufaa akahitimu elimu ya msingi, akafaulu kuendelea na masomo ya sekondari. Lakini kama ilivyokuwa kwa dada yake nae hakuwa na ada. Safari ya masomo kwa upande wake pia ikaishia hapo. Hii ni kwa vile kipato kidogo cha Ramla kilitosha chakula chao. Kodi na mtaibabu walipoumwa pamoja na nauli ya kumpeleka Ramla katika viwanja kusaka wanaume na kumrudisha nyumbani.
Mzimu wa mzee Mwinyihumbe ukiwatokea mara kwa mara ukiwasihi waendelee kupendana. Wakaendelea kupendana.
Halafu asubuhi nyingine ya siku nyingine isiyo na jina, ikaja. Ramla akarejea na mwanaume mmoja bonge la baba pandikizi la miraba mine. “Huyu ni mdogo wangu, anaitwa Shufaa” Ramla akamtambulisha .
“Na wewe Shufaa, huyu ni shemeji yako Anaitwa Samson Kidude. Mwenyewe anapenda kuitwa Sam. Tutakuwa nae hapa kwa muda kabla ya kulekea kwake Arusha!” Ilikuwa zamu ya Shufaa kutambulishwa. Kila mmoja akafurahi kumfahamu mwenzake. Walipobaki peke yao, Shufaa akasaili kwa shauku.
“He! Dada tunakwenda Arusha!! Kufanya nini?”
“Kuishi, Kidude ananipenda sana na amenihakikishia kwamba atanioa muda si mrefu”
Zilikuwa habari mpya na nzuri kwa Shufaa. Nzuri kwa maana ya kuishi kwa uhakika na na kumuondoa dada yake katika hatari ya kuambukizwa Ukimwi.
Hayawi hayawi huwa. Muda ulifika na hatimaye Ramla aliolewa. Wengi wa waliomfahamu vizuri wakabakia kushika vichwa midomo ikiwa wazi.
“Haa! Ramla kaolewa?! Ramla huyu huyu wa maji mara moja?” Walijuliza mara nyingi bila kuliona jibu la wazi lililokuwa mbele yao.
Ramla na Shufaa wakaiacha midomo hiyo wazi, wakatoka Zanzibar na kuhamia Arusha walikopokelewa kwa shangwe na familia ya Samson Kidude.

*          *          *
Arusha maisha yalikuwa mazuri mfano hakuna. Walipata kila walichohitaji, wakila na kulala mithili ya watawala wadogo wa nchi fulani. Bahati mbaya ilikuwa kwa Ramla aliyeishazoea kulala na wanaume watatu hadi wane kwa siku. Huyu mumewe mmoja aliona kama anamzingua, Anamgusa gusa tu na kumuacha na kiu yake.
Hii ilikuwa sababu iliyomfanya Ramla kutoka nje ya ndoa yake kutafuta kile ambacho alidhani hakukipata ndani ya ndoa. Mdogo wake alipogundua akamuweka chini na kumwambia afanyavyo sivyo. Ramla akamsikiliza tu kama muziki na kuahidi kujirekebisha. Hakujirekebisha!
Watu wakaviona vitendo vyake. Mumewe akasikia wee mwishowe akachoka. Akaandaa mtego uliomnasa Ramla vizuri sana.Akaumia sana na kama mwanaume akachukua hatua.
Ramla akaachika.
Akayazima pia matarajio ya mdogo wake ya kuendelea kusoma zaidi kwa kuwa walitimuliwa  katika nyumba ya Samson.
Kurudi Zanzibar ikawa haiwezekani tena.
Wangerudi vipi hali nauli yenyewe tu hawakuwa nayo? Shufaa alimlaumu sana Ramla. Ilikuwa kazi bure, maji yalishamwagika. Ikabidi Ramla arudi kwenye udada poa tena. Wakati huu mwili wa Shufaa ulishakatika kibantu zaidi na kupendeza sana ukiyavuta macho wa wengi kila alipopita.
“Shufaa mdogo wangu,” Siku nyingine Ramla alimwita, “Nimechoka kukulisha! Kipato changu ni kidogo sana, na isitoshe umeshakuwa mkubwa sasa. Tusaidiane kutafuta riziki sasa. Wateja wamekuwa wachache sana viwanja, hivyo jiandae kuanzia leo tutatoka wote sawa?”
“Dada niwe Malaya?!!” Shufaa akashtuka vibaya sana.
“Siyo Malaya mdogo wangu, Malaya hufanya ngono kwa kupenda. Sisi tunafanya biashara. Tunafanya kazi ili tuishi  sawa?”
Ilikuwa mfano wa amri. Japokuwa Shufaa alilalamika  na kumlilia dada yake bado haikusaidia. Siku kadhaa baadae Shufaa nae akaingia katika biashara ya kuuza mwili wake. akawa changudoa hasa. Alizunguka maeneo ya ICC, Ngarenaro, Majengo na katikati ya mji kama siyo jiji.
Ghafla muujiza ukatokea.
Shufaa alikuwa amemkoleza vilivyo Bwana Busara Hussein, mfanyabiashara mkubwa pale Arusha. Huyu akatangaza ndoa. Ikalazimu wakafungie kwa jirani yao kwa kuwa Shufaa, mbali ya Ramla hakuwa na ndugu mwingine. Shufaa akawa mke wa Busara Hussein.
Dada yake Ramla akawa haishi kuja kuomba omba misaada hii na ile kwa mdogo wake Shufaa akimlalamikia ugumu wa maisha na jinsi mabuzi yalivyoadimika.
Alipoona taabu za dada yake zimezidi, Shufaa akamuweka mumewe chini na kumuomba amruhusu dada yake aje kuishi hapo.
Akiwa amevishuhudia vitendo vya kihayawani vya Ramla, na akiwa tayari amelala nae mara kadhaa; Busara hakukubali Ramla aje kuishi nyumbani kwake. Alikataa kata kata.
Lakini unyonge wa kuendelea wa mkewe aliyempenda ukomo wa kumpenda ukamfanya abadili uamuzi. Siku chache baadae Ramla akaja pale , wakaishi wote. Shufaa alifurahi kupita kiasi. Mumewe akapewa penzi la hali ya juu.
Shetani ni shetani tu, ukimuweka kwenye chupa lazima tu atatoa kidole nje. Haikuchukua muda Ramla kuanza kumzoea Busara kwa nguvu, na haikumchukua muda tena  kumfanya Busara atoke nje ya ndoa yake na kutembea naye. Wa kwanza kuliona hili walikuwa watumishi wa ndani. Vile walivyompenda Shufaa wakamwambia kila kitu, akapuuza.
Mungu siyo Wamaywa siku moja Shufaa akawafumania Red Handed wakifanya ngono juu ya kitanda, ndani ya nyumba  na chumba chake! Akokosa hata ujasiri wa kuwafanya chochote, akaishia kulia!
Wakakiri makosa kwa dhati, wakaomba msamaha  wakiahidi kutorudia. Masikini ya Mungu Shufaa akawasamehe, yakaisha. Maisha yakaendelea.
Yakawa yale yale ya muonja asali kutoonja mara moja…

*          *          *
Halafu ikajiri siku nyingine tena! Siku hii ilimkuta Shufaa nje kidogo ya jiji akiwa ndani ya gari yake ndogo  Baloon Jeupe aliyoipenda.
“Shit!” Shufaa akagurta akiizungusha Baluni hii kwa fujo kurudi alipotoka. Vile alivyokuwa amependeza kwa rinda zuri jekundu na vile alivyoheshimika kama mke wa mfanyabiashara maarufu; Shufaa hakuona kama ni busara kubishana na walinzi wa kwenye ile Kitchen Party ya Shoga yake Hawa kwamba yeye ni mwalikwa halali ila tu amesahau kadi ambayo ingemuwezesha kuingia ukumbini.
“Shit!” Akaguta tena akizidi kukanyaga mafuta.

*          *          *
“Ujue una hatari wewe?” Ramla akasema  kwa sauti isiyo na upinzani wowote huku akivaa bikini yake. Busara alikuwa amemuomba wakaogelee nje kunako lao bwawa la kuogelea  baada ya kufanya mapenzi ya kukata na shoka toka Shufaa alipoondoka.
“Hatari gani honey?”  Busara akasaili akimkumbatia na kumpiga busu jingine la haja.
“Huwaoni walinzi na watumishi waliotapakaa huko nje, wakituona na kumwambia Shufaa je?”
“Achana nao mimi ndiyo bosi!”
“Na je mkeo akija na kutukuta?”
“Atajiju! Ujue wewe unajua mapenzi kumzidi, yeye akilala chali ni hivyo hivyo mpaka unabwaga mzigo wako wa kuni. Poh! Mwanamke gani yule,” Busara akamjibu wakitoka nje. Kabla hawajaifikia Swimming pool, Ramla akamuomba waketi kidogo kwenye kiti cha kupumzikia kabla ya kuogelea kwanza kwani kuna kitu muhimu alitaka kumwambia.
Shufaa aliwakuta hapa katika hali hii.
Yaelekea maongezi yalikuwa nyeti na matamu sana kwani mpaka Shufaa anaegesha gari yake, anashuka na kuwasogelea huku akiwa amepigwa na butwaa, hawakuwa wameshtuka mpaka alipowakaribia zaidi na kuwakurupusha.
Unadhani walimjali? Sana sana aliambiwa hajui mapenzi, hivyo mawili ama achague kufungasha virago vyake, kuachia ngazi na kurudi kwao. Ama akubali Ramla awe mke mwenzie, mke mdogo!.
“Poh!” Shufaa akatema mate kwa kinyaa na dharau. Bila kusema lolote akairudia Baluni yake mbio na kujipakia kwa hasira. Akaiwasha, akazungusha usukani kwa nguvu akiwa amekanyaga mafuta kwa nguvu zake zote. Gari ikaunguruma kama mtoto wa samba ikifyatuka kwa kasi ya ajabu. Almanusura aligonge geti. Lakini Mungu alimsaidia, akatoka salama na kutimkia kwa Mwayaona Biti Kuishiwa…

*          *          *
“Nyamanza Shufaa! Nyamanza Mwanangu!” Mwayaona akasema baada ya kuisikia historia ya Shufaa na Ramla. Kifikia hapo Shufaa alikuwa hajiwezi kwa kilio. Akaendelea kumbembeleza.
“Wewe ni Muungwana Shufaa. Na siku zote Muungwana akivuliwa nguo huchutuma! Dada yako kakufanyia ushenzi wa kukuvua nguo, muache aende nazo. Wewe chutama. Watatokea waungwana wenzako na watakupa nguo nzuri kuliko zile za awali! Umesikia?”
Shufaa akatikisa kichwa chini na juu kuafiki.
“Kama hivyo ndivyo, basi usihuzunike sana na maadamu mimi shoga yako nipo huna sababu ya kudhalilika kiasi hicho. Wewe nenda kachukue kila kilicho chako uje tuishi wote hapa tukitafakari nini cha kufanya. hakuna dharau mbaya kama aliyokufanyia Ramla. Mwache apate yeye!”
“Ahsante sana mama, wacha nifanye hivyo!” Shufaa akainuka na kutoka akiwa amefarijika sana.
Kabla hajalifikia gari yake, akasikia honi kali. Alipotazama nyuma akaiona Toyota Land Cruiser VX ikitafuta parking mkabala na nyumba ya Mwayaona. Akaidharau na kufungua mlango wa Baloon.
“Shufaaaah!!” Akaitwa kwa nguvu  Akageuka.
“Mungu wangu!” Shufaa akamudu kutamka. Aliyemwita alikuwa Hamis Abdalaah, yule kaka yake wa hiyari, ambaye wakati msiba wa Mwinyi humbe unatokea yeye alikuwa India. Kaka ambaye alimpenda kupita kupita kiasi, kaka aliyekuwa kimbilio lake.
Shufaa akatabasamu. Haitoshi kusema moyo wa Shufaa uliripuka kwa raha, haitoshi kusema hakutegemea, haitoshi kusema…! Alijikuta akimkimbilia na kumkumbatia kwa nguvu zake zote kilio kikimunguka upya.
“Jamani kaka… Kaka Hamis. Kaka Magic” Akaweweseka akilia kifuani kwa Hamis
“Nilishawatafuta mpaka basi!” Hamis akalalama akimpigapiga Shufaa mgongoni kwa upendo. Shufaa akalia zaidi na kumsimulia kaka yake mkasa mzima wa yeye na dada yake Ramla.
Never mind” Hamis akamfariji. “Twende zetu Zanzibar. Kuna kila kitu mdogo wangu. Fadhila za Mzee Maulid Mwinyihumbe kunipeleka India, nitazilipa kwa kukutunza wewe, nikianza na kukusomesha!”
“Kweli kaka?”
“Mungu mmoja vile. Hukustahili kuolewa mapema hivi ungali unahitaji kusoma!”
“Nitashukuru kaka!”
Ukimya mfupi ukapita. Shufaa akauvunja kwa kuuliza. “Na wewe ulifanikiwa vipi kaka, naona mambo yako siyo mabaya.”
“Ni kweli mambo yangu ni mazuri sana namshukuru Mungu. Nilivyofanikiwa ni hadithi nyingine ndefu, wewe twende tu nyumbani nitakueleza kila kitu”
Shufaa akamshukuru Mungu.
Alipotaka kuondoka akaitazama funguo ya Baloon yake na kuitazama gari yenyewe. Akamgeukia Hamis na kumwambia “Samahani!” Halafu akamrudia Bi. Mwayaona mbio na kumrushia zile funguo.
“Za nini?” Mwayaona akauliza akizidaka
“Ya lile gari pale, nimekupa! Mimi naende Zanzibar kusoma! Kaka yangu amerudi toka India!”
“Wewe!!!” Mwayaona akaripuka kwa furaha “Sema kweli?”
“Haki ya Mungu. Gari lile ni mali yako”
Mwayaona akashukuru kupita kiasi. Shufaa akamuacha akirukaruka, akaingia ndani ya gari la Hamis na kutokomea kwenda Dar es Salaam na baadae Zanzibar kuanza maisha upya.


MWISHO

Maoni ushauri wasiliana nami katika 0755 697 335 au baruapepedhahabugroup@yahoo.com

No comments:

Post a Comment