Na Hussein Wamaywa
Wakaashusha pumzi nzito wakitazamana kama wanaotegeana nani aongee. Tausi akawatazama tena watu hawa na kushindwa kuwaelewa. Kushindwa kuwaelewa kwa maana ya kuelewa kilichowaleta. Wasiwasi uliwazingira, hofu ikiwaangukia na woga kuwatawala. Hali iliyopelekea moyo wa Tausi kuanza kuzingirwa na hofu pia.
Mjomba mtu akakohoa. Wote wakageuka kumtazama.
“Labda niwaletee vinywaji mpoze makoo kwanza! Pengine mmechoka na safari!” Tausi alikuwa amekumbuka kuwaambia hivi baada ya kuona kujikanyaga kwa wageni wake hawa kumezidi.
“Hapana!” Yule ambaye siku zote amekuwa akimtambua kama kaka mkubwa wa mchumba wake Junior, akakataa.
“Lakini si tungekunywa tu, mimi nipe pepsi!” Maisara ambaye ni mpwa wa Junior na mtu aliyezoea kumtania Tausi kila mara akapinga.
“Huu si wakati wa kunywa na kuburudika Mai, ni wakati wa kuketi na kutafakari!” Alikuwa Shangazi wa Junior kwa upole na masikitiko. Akaendelea kusema, “Kutafakari mustakabali wa maisha yetu!”
Tausi akazidi kushangazwa “Wana nini watu hawa leo?” Akajiuliza. Hakupata jibu.
“Sasa si mmwambie tu watu tukaendelee na shughuli zingine. Kwani mkikaa kimya habari hazitomfikia? Maisara akasema kwa karaha.
“Kwani kuna nini? Niambieni mnitoe katika hofu jamani, naweza kufa kwa kihoro kabla ya siku zangu!” Ilikuwa kauli ya utani toka kwa Tausi.
Lakini hakuna aliyejaribu walau kutabasamu wachilia mbali kuonyesha meno na kucheka. Hata Maisara? Tausi akawaza na kupata hofu zaidi.
“Baba Shemsha!” Shangazi Zaituni akamwita mumewe. Yule aliyeonekana mjomba wa Junior. Mjomba Farouck akamtazama mkewe katika namna ile ile inayoweza kutoa jibu la unasemaje.
“Lakini ninyi ndo wanawake wenzake. We mueleze tu, atakavyowaeleza ninyi ni tofauti na atakavyonielewa mimi!”
“Wanawake wenyewe tuko wangapi hapa? We mueleze tu!
Tausi pia akamtazama mjomba wake huyu kwa namna inayosihi na kubembeleza aelezwe. Akajiandaa kueleza macho ya wote yakiongozwa na Tausi yakimtazama.
“Tausi mama!” Sauti yake ilikuwa ndogo, nzito na iliyosheheni upendo.
“Bee?”
“Wewe sasa ni mtu mzima mama siyo?!” Akasafisha koo tena.
“Ndiyo!”
“Mtu ambaye waweza kupokea jambo lolote katika ukubwa wake liwe baya au zuri siyo?”
“Ndiyo!”
“Tena mwenye kichwa kipana kinachopokea taarifa zote kuzichuja bila kutaharuki na baadae kuchukua uamuzi wa busara au nakosea Tausi.!”
“Acha kuzunguka mjomba!” Tausi akasema kwa karaha “We sema kitu kilichokuleteni basi. Kwani we hujui mi ni mtu mzima?”
“Tuliza munkari Tausi ujue…!”
“Niambie mjomba!”
“Kabla sijakuambia uniahidi kitu kimoja!”
“Kitu gani?
“Kwamba hutachukua hatua za kipumbavu pumbavu!”
Tausi akashtuka tena, Junior anataka kuoa mwanamke mwingine nini? Au ndo wameniona mi sifai kuwa mkwe wao na mke wa mtoto wao? Sasa wanataka wanirudishe kwetu kijanja? Bado hatujapata jibu.
“Hatua za kipumbavu pumbavu?!! Ndo hatua gani hizo? Ni kumdhuru Junior? Au huyo mkewe mpya?!! Au kujidhuru mimi mwenyewe halafu nini?!! Nitaishi vipi bila Junior ubavu mwangu?
Bila ya kusikia sauti ya Junior mpenzi initiayo raha na furaha? Bila vitendo vyake vinisisimuavyo mwili wangu kwa staili ya aina yake na kunipa raha? Bila kauli yake ifafanavyo na sauti ya zeze sikioni mwangu, ile yenye uzito wa besi lakini nyepesi kama ute wa yai iingiavyo vyema na kutuama chini kabisa ya moyo wangu?
Bila sura yake mwanana iliyobeba ndevu changa na tabasamu laini zuri ambalo kwalo pekee huwa burudani na tiba tosha kwa moyo na akili iliyochoshwa na vurugu za mchana na kutwa nzima. Bila penzi lake moto moto linitoalo katika dunia hii na kunipeleka katika ulimwengu mwingine?! Hapana! Hapana!! Akakataa kwa dhati.
Yeyote atakayenipokonya Junior wangu, Junior my Love, itambidi ahakikishe kwamba nimelala kwa utulivu chini ya ardhi, futi sita za mchanga au udongo zikiwa juu yangu ndipo apate fursa ya kumtwaa kiulaini kama…”
“Tausi?” mjomba akaita akijaribu kuvaa furaha bandia. Hakufaulu!
“Tafadhali nihakikishie kama hutachukua hatua za kipumbavu!”
“Na…Naa…Naku…Naku…!” Akashusha pumzi kwa nguvu.
“Niambie kwanza mjomba!” Akasema kwa jazba na karaha.
“Nitakuambia, lakini naomba uniahidi kwanza!”
“Nakuahidi!”
“Uniahidi mimi mbona humalizii?!
“Nakuahidi kwamba sitachukua hatua za kipumbavu na kijinga. Ninakuahidi pia kuwa mtulivu wakati wote wakati huo huo nikitafakari wa mapana yote uliyoniambia. Tena nikimuomba mungu anipe utulivu wa moyo na fikra mpya! Haya niambie sasa!” Akanitimisha.
Yalikuwa maneno ya ujasiri ambayo kwa wengine walioambatana na Ba’Shemsa hapo nyumbani kwa Junior anapoishi Tausi yalikuwa yamewagusa mioyoni hasa na kuwaongezea simanzi. Baadhi walihisi machozi yakitaka kuwatoka. Haraka wakainamisha nyuso zao chini ili Tausi asiwaone.
Maneno ambayo Tausi alikuwa ameyatoa tu ili aweze kuelezwa kile kilichomo moyoni mwao ambacho pia ndicho kilichowaleta hawa wageni hapa kwake hasubuhi hii na mapema. Nadhani itakuwa sahihi kusema yalitoka kinywani na si moyoni.
Moyoni kulikuwa na kauli moja tu ya siri ambayo haikuwa dhahiri.
Kwamba yeyote atakayejaribu kumpokonya Junior wake basi cha moto atakiona. Tena atakiona kwa maaana halisi ya kukiona na sio vinginevyo. Ba’ Shemsa akakaa vizuri na kusema.
“Kama nilivyotangulia kusema awali, wewe ni mtu mzima sasa. Tena mwanamke wa shoka. Mwanamke aliyepitia vingi na mengi mpaka kufika hapo ulipo. Sina shaka ni mwanamke jasiri, hata hili nikuambialo utalipokea kwa uzito unaostaili!” Akatua kumeza mate.
Wote wakimwangalia, Tausi alimwangalia kwa shauku zaidi.
“Ni sawa na kusema alopanga Mungu binadamu awezi kupangua. Junior hatunaye tena duniani!! Ame…!” akakatishwa na mlipuko wa kilio kutoka kwa Tausi. “What Ucle?!! Noooooooh...!”
Yalikuwa maneno machache tu ambayo Ba’Shemsa na wenzake hawakupata hata nafasi ya kutoa majibu ya kumfariji, kwani aliyasema kwa mstuko mkubwa mwili umemkakamaa kama aliyeshikwa na degedege, halafu akalegea ghafla, mlegeo ule wa unaoshinda mlenda kabla hajaangukia jiko la umeme lililokuwa limeinjika maji ya moto kwa ajili ya chai wakati huo.
Kabla hawajapata wazo la kumshika tayari maji yalishatenguka na kumwagikia katika bega la kulia, usoni na shingoni, halafu akaanguka chini na kuzirai. Matendo yote hayo yalifanyika kwa haraka sana ndani ya nukta mbili au tatu tu!
Wakati wenzake wanapata akili ya kumshika tayari maji yalishamuunguza vibaya sana. Heka heka za kumnyanyua na kumpeleka Hospitali zilifuata. Walikuwa wamekwisha chelewa.
* * *
Ghafla kukawa kimya. Zile kelele za muziki, maongezi ya bashasha honi na kadhalika vikawa vimekatishwa ghafla. Mshindo mkubwa ukasikika. Mshindo ambao haukuwa tofauti sana na ule wa silaha ya kurushia makombora ya kutungulia ndege, kuharibu majumba marefu na makubwa na kufanyaa maangamizi ya halaiki ukiwa umezizima kelele zote mithili ya kibatari kizimwavyo na upepo mkali.
Ukimya wa kuogofya ukatawala kwa sekunde mbili tatu.
Halafu vilio vya “Mama nakufa!! Ooh! Yesu Kristo Masiha!! Msaada tunaangamia!! Tuokoeni Yalarasulilahi!! Ooh! Yesu Kristo Masiha!! Tenda miujiza sasa!! Tuombee kwa baba tunakufa!! Mama Ooo!!Mayee!!” Vikafuatia. Na kadiri muda ulivyokwenda ndivyo vilio vilivyoongezeka.
Glafla Junior akazinduka. Tumepata ajali! Akasema akajaribu kuinuka akajigonga kwa juu na kabla hajakaa sawa akajigonga tena, wakati anarudi chini ili ajiandae kutafakari upya akateleza na kuanguka.
Alipotazama kilichomfanya ateleze, akaogopa. Damu! Akainua macho kutazama kule ilikotokea.
Hakupaona mara moja, lakini ilikuwa ikimminika taratibu mithili ya maji yatokanayo katika mashine ya kukamulia juisi wakati juisi ikikamuliwa.
Akataharuki na kwa kutumia mlango wa dharura Emergency door; akafaulu kutoka nje. Akapumua kwa wasiwasi kelele za wenzie ndani ya gari hilo basi lililolala kitulivu kichwa chini miguu juu; zikimtia hofu, wasiwasi na kumnyima amani moyoni.
Wazo likampata akaitoa simu yake ya mkononi akapiga 112 kuomba msaada. Japo ilimchukua muda kusubiri ahudumiwe, lakini badae alihudumiwa. Akakata simu kwa faraja na kusubiri kwa matumaini akijua msaada u’karibu unakuja.
Ghafla akakumbuka kitu. Tausi Msafiri, yule mwanamke mrembo na mcheshi aliyeifanya safari yake hii ya kutoka Dodoma kuelekea Morogoro na baadae Tanga iwe fupi na tamu kupita kiasi hakuwemo! Upesi akarudi ndani ya gari. Alifaulu kumuona Tausi akiwa amebanwa na chuma Fulani miguuni.
Naye kama walivyo abiria wengine wengi, alikuwa akipiga kelele kwa uchungu.
Akajikusuru kumuokoa. Haikuwa kazi rahisi. Tausi alipiga kelele za maumivu kwa wakati wote Junior alipokuwa akijitahidi kumuokoa mpaka alipopoteza fahamu. Junior akaendelea na juhudi za kumnasua.
Mara watu kutoka kijijini wakawasili na harakati za uokoaji zikaanza kwa ushirikiano, wengine walipora kila walichoona kina maslahi. Kwa msaada wa watu hawa, Junior alifaulu kumnasua Tausi. Aliweza pia kuipata mizigo yake miwili kati ya mitatu aliyokuwa nayo na kuanza kuilinda.
Akamtenga mbali na halaiki akimpepea na kumpa huduma ya kwanza.
Muda mwingi baadae ndipo gari lililowaleta waokoaji likawasili na kukutwa kazi ya uokoaji ishafanywa na mseto wa raia wema na wabaya. Kazi yao ikawa moja, kuwabeba majeruhi na kuwapeleka hospitali iliyokuwa jirani!
Bado Tausi Msafiri alikuwa amezirai!
Junior alikuwa ameumia kidogo sana kwa maana ya kukatika kidole chake kidogo cha mkono wa kushoto. Kilikuwa kimekatika juu kidogo ya ukucha. Maumivu aliyonayo hayakuwa makali kama yale ya Tausi. Akaamua kukaa na kumuuguza kwanza.
Wiki mbili baadae Tausi alitoka hospitali akiwa hawezi kutembea mwenyewe. Alikuwa akitembelea baiskeli kama mlemavu wa miguu.
Daktari alikuwa amemueleza kwamba atachukua muda mrefu kupona kwa kuwa vile vyuma alivyowekwa miguuni, vitapunguza uwezo wa asili wa miguu katika kubeba kiwiliwili.
Wakati wako Dar es salaam, pale anapoishi Junior, Tausi alikuwa akilia kwa uchungu, uchungu wa kumlaumu muumba na kukata tamaa akiamini mwisho wa maisha yake umefika. Alilia mno, alilia kupita kiasi.
Kilio kilimtia simanzi Junior, nae akaungana nae kulia kumya kimya. Alilia kwa muda mrefu na alipochoka alifuta machozi akamsogelea na kumwita taratibu
“Tausi…Tausi! Basi…, usilie sana inatosha Tausi. Ukilia sana utamkufuru mungu…!”
Tausi akageuka na kumtazama Junior akajitahidi kunyamaza bila mafanikio. Akaishia kusema hivyo hivyo. Msemo uliotawaliwa na kilio.
“Acha nilie Junia…acha nilie ndugu yangu. Kila siku mwenendo wa maisha yangu unaelekea katika hasi badala ya chanya. Wazazi wangu sikupata hata bahati ya kuwaona, nimeishi bila ndugu katika manyanyaso ya hali ya juu.
Mpaka nilipopata mchumba ambaye aliyenipenda na akaamua kunipa mtaji huu. Leo mtaji umepokonywa ajalini, miguu nayo imepokonywa ajalini uzuri wangu nao umepokonywa. Nani atanipenda nikiwa kiwete Junior?!” akalia zaidi.
“Usiseme hivyo Tau, wapo walemavu wengi waliofanikiwa kupita hata watu wazima. Isitoshe wewe sio mlemavu. Daktari kasema itachukua muda kidogo mifupa iliyobonyea kuungana na kupata nguvu. Kwa hiyo alichosisitiza ni mapumziko ya muda mrefu.!”
“Acha kunifariji Junior, hizo ni faraja tu. Daktari ana saikolojia.
Oooh! Mungu wangu kwa nini hukuchukua roho yangu siku ile ulipoichukua miguu yangu?” Akalia zaidi.
“Basi usilie sana!” Junior akambembeleza nae akalia machozi.
Walilia na kulia mpaka walipochoka na kupitiwa na usingizi.
* * *
Safari hii walikuwa wamesafiri pamoja tena. Walikaa mbele sambamba na dereva na walimfokea kila alipozidisha mwendo. Hatimaye walifika Dodoma, wakabadili gari na kupanda Hiace. Safari ya kuelekea Kondoa alikozaliwa Tausi ikapamba moto. Ingawa Dereva wa gari kubwa walikuwa wamefaulu kumdhibiti, dereva wa Hiace walishindwa kumthibiti.
Mara mbili alisimamisha gari na kuwataka washuke kama hawaridhiki na mwendo wake. Kwa kuwa magari yalikuwa haba, wakalazimika kusafiri hivyo hivyo mioyo yao wakiwa wameikabidhi kwa mungu. Tausi alisali mfululizo toka safari inaanza mpaka wanafika.
Walipokelewa na baadhi ya jamaa na marafiki zao.
Wengi walitokwa na machozi kuona Tausi akirejea katika kiti chenye magurudumu. Aliposimulia ilivyokuwa wengi walilia zaidi. Hii ikazidi kumchoma na kumuumiza moyo. Naye akaanza kulia. Alilia mno, alilia kupita kiasi.
Bahati nzuri Junior alikuwepo, na alihakikisha anakuwa na faraja ya kweli kwa Tausi. Hatimaye walifika nyumbani kwa Tausi na mtu akatumwa kwenda kumwita Fadhili mchumba wa Tausi aliyempa mtaji.
Fadhili alifika mbio akitweta. Habari za mchumba wake kurudi akiendeshwa katika baiskeli ya miguu minne, zikiwa zimemfanya achapuke mbio. Pumzi zilimtoka taratibu, alimwangalia Tausi aliyekaa pembeni mwa kijana yule mzuri ambaye ndio kwanza alikuwa ametoka kumfuta machozi.
Hisia za wivu, chuki, uchungu na dhana za kuibiwa zikatawala alichoweza kusema kwa wakati huo ni kusema “Asante sana Tausi!” mikono ikitetemeka kwa hasira.
Tausi akaangua kilio!
* * *
Alikuwa kitandani pale Hospitalini, fahamu zilianza kumrejea kidogo kidogo huku historia ya uhusiano wake na Junior ikirejea taratibu kama anayeota ndotoni.
Alikumbuka Junior alipokuwa pamoja na yeye wakati wa Fadhili alipoondoka nyumbani kwao kule Kondoa. Akakumbuka pia jinsi walivyoita wazee na kuwaeleza kilichotokea, wazee wakamtafuta Fadhili na kumuweka kitako.
Ambapo alisema Tausi amemkosea heshima na adabu licha ya kumtoa katika mikono ya mama wa kambo alipokuwa akimtesa hujaona. Akamtolea mahari baada ya kumuhurumia pale aliposikia mateso anayoyapata.
Kama kwamba hiyo haitoshi akampa mtaji wa kutosha ili asibweteke kwa kutegemea fedha za mchumba pekee. Mtaji huo ulimwezesha kutoa bidhaa Dodoma ambazo hazipatikani kwingine kokote na kuzipeleka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.
Kisha akatoa bidhaa za kule, ambazo nazo hazipatikani Dodoma. Sio siri kwamba biashara hii iliyainua maisha ya Tausi na kama shukrani yake Fadhili, aliapa kumpenda kwa dhati, kumuheshimu na kuwa mwaminifu wa kweli katika ndoa yake wakati wa kuolewa utakapojiri.
Fadhili aliendelea kulalama kwamba Tausi amekuwa hamjali, hampendi wala amthamini kiasi cha kufikia hatua ya kumletea mabwana kwa kisingizio cha marafiki ili awaone na ajue kwamba hayupo peke yake.
Alipiga hatua kubwa zaidi pale aliposhindwa kuamini kama Tausi amepata ajali kweli, kwamba anajaribu kumwongopea kwa kutumia baiskeli ya walemavu! ”Ujanja wa kitoto huo!” alihitimisha hivyo na kusimama tayari kwa kuondoka.
Wazee wakamzuia na kumuliza ni kwanini haamini kama mwenzie amepata ajali? Akajibu kwamba huwa anasikiliza redio, kuangalia TV na kusoma magazeti kila siku ya Mungu. Lakini katu hajasikia ajali yao kutangazwa redioni, gazetini wala katika TV!”
“Usiwe mpumbavu? Mzee mmoja akatamka kwa hasira na kuendelea.
“Wenzako huwa wanapima kwa kuangalia vyeti vyenye ugojwa, jina na mihuri
ya hospitali husika!”
“Mimi sio mpumbavu baba. Kufoji kitu katika Tanzania kama una fedha ni kiturahisi kama kuvunja biskuti. Kama wameza kupata kupata baiskeli ya mlemavu cheti na muhuri kitawashinda nini?! Nishasema mimi na yeye basi basi!! Nataka tu mahari yangu tena anipe sasa hivi mbele yenu!” Povu la hasira likamtoka.
“Fadhili?!! Hivi umerogwa au?”
“Bado tu hamuamini nisemacho? Subiri muone” Akamaliza na kuinuka akamfuata Tausi pale kitini, magongo yake akayasukumia kando kisha akamshika kifuani “Mtamuona amesimama mwenyewe!” Akamwinua kwa nguvu na kumuacha kasimama. Akarudi kitini kwake na kuketi.
Maumivu makali ambayo hakuwahi kuyasikia kabla yakaivamia miguu na mwili wa Tausi. Akaanguka chini akilia kwa maumivu kwa sauti kuu. “Si mmemuona...?!” Fadhili akabweka katikati ya kilio cha Tausi na kuendelea “Kusimama anaweza kabisa asituzingue kwa kilio na baiskeli. Huyu ni mwongo kabisa!!”
Junior ambaye alikuwa kimya muda wote akisikiliza kila neno kwa masikitiko makubwa, alishindwa kabisa kuzihimili hasira zilizomjia ghafla akainuka na kufyatuka kama mshale mpaka kwa Fadhili. Akamuinua kama unyoya na kumbandika vichwa kadhaa vya usoni.
Akamtuliza kwa kumsukumizia makonde mengine kadhaa ya haja kabla hajamuachia akianguka chini kama gunia la sufi huku sura yake ikiwa haitamaniki. Ikiwa haitofautiani pia na lililotumbuka vibaya vibaya (Masalo). Akafungua pochi lake, akatoa bulungutu kubwa la fedha na kumpiga nalo usoni. Akawafuata wazee wale na kuomba radhi kwa kitendo kile.
Akatoa taarifa kwamba zile ni fedha za mahari anayodaiwa Tausi na Fadhili, Halafu akamnyanyua Tausi na kumpeleka hospitali. Siku chache baadae uchumba wa fadhili na Tausi ukavunjika rasmi.
Badala yake ukazaliwa uchumba mwingine wa Tausi na Junior. Halafu wakaondoka Kondoa na kurudi Dar es Salaam.
* * *
“Usiwe na wasi wasi mpenzi! Kama wapo wasioiona thamani yako wengine tunaiona. Ajali ile sikuisababisha mimi, lakini tumekuwa pamoja toka ajali ilipotokea mpaka sasa. Kitendo cha mchumba wako kukutema kwa ajili yagu kimenigusa kupita kiasi. Naahidi kuwa nawe mpaka kifo kitakapotutenganisha!”
Hii ilikuwa kauli ya Junior kwa Tausi mara kwa mara.
Mara zote ilitoka kwa hisia za hali ya juu, hisia ambazo zilimgusa vyema Tausi naye akawa hana anachoahidi zaidi ya uaminifu na pendo la dhati kwa mchumba wake huyu.
Hili lilikuwa moja, lakini Junior alifanya kila aliloweza kuhakikisha Tausi anapona miguu. Aliazima, akakopa akaiba, akanyang’anya, akaongopa na kulaghai hata akapata kitita cha kutosha kilichowezesha Tausi kwenda kutibiwa London Uingereza.
Miezi mitatu baadae alirejea akiwa anatembea! Alimshukuru Junior kwa kiwango ambacho huwezi kukifikiria. Akampa mapenzi na mahaba mazito hujaona. Shukrani za dhati kutoka chini kabisa ya fungate la moyo wake zilimtoka kila mara.
Ingawa heka heka hizi za kutafuta fedha za matibabu ya Tausi zilimfanya afukuzwe kazi pale Dhahabu Publishers Co. Ltd kwa kusababusha hasara kubwa akiwa Markerting Officer; Junior hakujali, badala yake alizipokea shukrani hizi kama shujaa aliyerejea nchini baada ya kushinda vita.
Kilichofuatia walianza kuishi pamoja wakitafuta kazi kwa Junior kwa bidii. Mungu bariki wakawa wamefaulisha Junior kupata kazi kama dereva wa magari makubwa yaliyokuwa yakienda Mikoani kupeleka bidhaa na kuleta nafaka.
Tpripu mbili tu zikawafanya watabasamu.
Marupurupu na mshahara vilikaribia kuwafanya wawehuke kwa furaha. Yalikuwa mengi mno! Mengi sana. Walipanga vingi na mengi ambavyo wangevifanya kufuatia mapato ya kazi yao hiyo mpya. Lakini kubwa lilikuwa ni kufunga ndoa ya kifahari mara tu atakakapokwenda tripu ya kumi.
Kwa mahesabu yao, wangekuwa na shilingi milioni tatu, kujumlisha na akiba yao iliyo benki, wangeweza kufunga ndoa ambayo ingeacha historia ya kukata na shoka kama sio kuwaacha vinywa wazi wale wenzangu na mie wasiopenda kuona mambo ya watu yakifanikiwa!
Mara ya mwisho alikuwa ameenda tripu ya saba na alikuwa amechukua siku tatu akiwa safarini. Ilibaki siku moja tu arejee.
Na zilibaki tripu tatu tu zitimie tripu kumi wafunge ndoa; ndipo walipokuja mawifi, mashemeji maanti na maanko katika nyumba ya Junior na Tausi na kumpa habari za kifo cha Junior.
Naam! Junia ambaye ameweza kumrejeshea furaha yake iliyotaka kupotezwa na Fadhili, Junia ambaye alilia pamoja nae katika ajali iliyomsababishia ulemavu wa muda na kuwa kisa cha yeye kutemwa na Fadhili;
Junia ambaye alifanya kila alichoweza, ameiba na kuitoa hata senti yake ya mwisho ili kuhakikisha Tausi anarejea katika uzima; Junia ambaye amefukuzwa hata kazi kwa ajili ya Tausi! Junia mabae…Junior ambaye….!”
Ndio kwanza fahamu zikamrejea sawa sawa akipambazukiwa na ukweli kwamba Junior wake mpenzi alikuwa hayupo tena duniani. Alikuwa amefariki! Amefariki na kumwacha Tausi peke yake akiwa hana mbele wala nyuma.
Akaangua kilio kidogo pale kitandani.
Mjomba wake akambembeleza “Ndiyo hali ya dunia Tausi. Kilichopangwa na muumba binadamu hawezi kupangua. Sote ni wa mwenyezi mungu na kwake tutarejea. Acha kulia usije mchukiza mwenyezi mungu!
Zilikuwa nasaha kutoka kwa mjomba. Tausi akapunguza kasi ya kilio na kunyamaza baada ya kusina sina kwa muda.
“Kitu gani kimemuua mchumba wangu?” Akasaili baadae
“Ajali ya gari. Amegongana uso kwa uso na fuso iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kuelekea Iringa. Ni bahati mbaya kuwa wote wamefariki. Hakuna aliyepona katika magari yote mawili. Ilikuwa ajali mbaya sana! “Akatua, Tausi akianza kulia kimya kimya tena.
Mara daktari akaingia. Wakamsihi tausi anyamaze, akanyamaza.
“Mwili wake upo wapi?” Tausi akakaidi amri ya kukaa kimya.
“Mochwari! Hapa hapa hospitali!”
“Hii ni hospitali gani?”
“Muhimbili!”
Tausi akajiinua kitandani na kutaka kushuka. Daktari akamzuia
“Unakwenda wapi?”
“Mochwari! Nataka kuuona mwili wa Junior wangu!”
“Haitawezekana bado unaumwa, Tausi pumzika!”
“Nimeshapona niacheni!” Akachachamaa akishusha miguu miwili chini
“Maiti imeharibika sana Tausi, isitoshe haitazikwa kabla hujatoa salamu za mwisho pumzika Tausi bado una maumivu makali.
“Sina maumivu Dokta! Mi ndo’ mgojwa. Tafadhali sana naomba niuone mwili wa mume wangu japo…japo kichwa tu nitaridhika. Ukweli siwezi kulala kama hamtoniruhusu kufanya hivyo!”
Machozi yakawa yakimtoka.
Daktari na ndugu wa Junior wakatazamana. Daktari akabetua midomo na mabega kwa pozi! “Je” Mjomba akasaili “Kutakuwa hakuna tatizo kama atakwenda sasa hivi?”
“Midhali mwenyewe kasema anaweza, fine mpelekeni. Ujue tiba huwa inafanya kazi pamoja na fikra na hisia za mgojwa. Mnaweza kumpeleka akauone mwili wa mumewe!”
Nesi akaitwa. Akaichomoa drip ya maji, wakamwinua Tausi na kuziweka vizuri bandeji alizofungwa usoni. Shingoni na mabegani. Wakamfunga kanga vizuri, safari ya kuelekea mochwari ikaanza, Tausi akisali kimoyo moyo!.
“Dear Junior, usifadhaike kwa kuniacha ghafla pasipo kunipa japo busu la kuniaga. Najua hukupenda iwe hivyo bali kulingana na sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wako umeshindwa!.
Sikulaumu kwa hilo. Hata ningekuwa mimi ningefanya ulivyofanya. Pole kwa safari yenye maumivu kuelekea huko katika ufalme wa Mungu.
Nasema usifadhaike. Usifadhaike kwa sababu hutaishi huko peke yako walau kwa siku mbili tu. Ndani ya siku moja au mbili nitakuwa nimefika na tutaishi pamoja katika bustani ya Adeni. Ile ambayo baba yetu Adamu na Mkewe Hawa kama sio Eva walikuwa wakipumzika.
Nafanya hivi ili tu kutimiza ile ahadi ambayo nimeitoa mara nyingi tukiwa pamoja, mara nyingi baada ya kufanya mapenzi. Kwamba siwezi kuishi bila wewe walau kwa siku moja tu. Pumzika, pumzika kwa amani Junior, Tausi ni njiani ninakuja.
Ninachofanya sasa ni kwenda kuuona mwili wako uliohifadhiwa mochwari. Nikitoka huko nitashiriki mazishi yako kisha nami nitakufuata kwa kunywa sumu ya…!”
Tausi akaikatiza sala yake ghafla. Walikuwa wamefika mochwari. Mjomba wake akaongea na muhudumu wa mle kwa muda, kabla muhudumu yule hajageuza uso na kumtazama Tausi. Kisha akafungua mlango na kumwita. Wakamfuata mioyo yao ikiwadunda kwa hofu.
Waliingia wakiwa na mawazo ya kuona mlundikano wa maiti zilizolala zigi zaga bila mpangilio maalum...
MWISHO